Makubaliano ya Kuendesha Kozi ya Diploma ya Sheria kwa Kushirikiana na Chuo Kikuu Mzumbe Morogoro

Mkuu wa Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Tanzania SACP. Willington Kahumuza na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha wamesaini hati ya makubaliano yanayolenga kuanzisha na kutoa Stashahada ya Sheria baina ya vyuo hivyo tarehe 12/06/2024. Aidha katika hafla hiyo Mkuu wa Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Tanzania (TCTA) SACP. Willington Kahumuza amesema ni fursa kwao kuimarisha ushirikiano utakaoleta tija baina vyuo hivyo kwa watumishi kubadilishana uzoefu lakini pia kuhakikisha wanafunzi wanaohitimu wanakuwa wabobevu na kuweza kukidhi mahitaji ya jamii katika masuala ya sheria.
Makubaliano ya ushirikiano huu yanaelekeza ushiriki wa Chuo Kikuu Mzumbe katika kuandaa mitaala, usimamizi na uandaaji wa mitihani na kisha kutoa vyeti kwa wahitimu wa Stashahada hiyo. Pia, ushirikiano huu unaelekeza Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Tanzania (TCTA) kutoa miundombinu itakayosaidia wanafunzi kupata taaluma kwa kuzingatia mtaala.